2 Juni 2025 - 20:16
Source: Parstoday
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akutana na Rais wa Misri jijini Cairo

Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana leo Jumatatu na Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri jijini Cairo.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Alam, Araqchi aliwasili mjini Cairo jioni ya Jumapili kwa ajili ya mashauriano na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Misri.

Katika ziara hii, Araqchi amekutana na Badr Abdel Aati, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, pamoja na Rais Abdel Fattah El-Sisi kwa ajili ya kujadili hali ya sasa ya uhusiano wa pande mbili na masuala ya kikanda, hususan umuhimu wa kukabiliana na jiniai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina, pamoja na baadhi ya masuala ya kimataifa.

Ismail Baqaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, alitangaza ratiba ya Waziri wa Mambo ya Nje ya kutembelea Misri na Lebanon alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi jioni.

Akizungumzia juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuimarisha uhusiano na ushirikiano na mataifa ya eneo, Baqaei amesema: “Safari ya Araqchi nchini Misri na Lebanon inalenga kujadili mahusiano ya pande mbili na kufanya mashauriano kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo, hususan hali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, pamoja na matukio ya kimataifa.”

Baqaei amesema kuwa ziara ya Araqchi nchini Misri na Lebanon inaendelea leo Jumatatu na kesho Jumanne, ambapo anatarajiwa kukutana na viongozi waandamizi wa Misri na Lebanon ili kujadiliana na kubadilishana nao mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya pande mbili na ya kieneo.

Your Comment

You are replying to: .
captcha